MKUU wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo ameagiza ifikapo leo, wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo, wawe wamewapa zawadi zao watumishi bora wa mwaka huu baada ya kubaini walitoa zawadi hewa kwenye sherehe za Mei Mosi.
Ameagiza
pia Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Pwani pamoja na mkurugenzi wa
Shirika la Elimu Kibaha, nao kutoa zawadi ya fedha kwa wafanyakazi
waliofanya vizuri kwenye vitengo vyao, badala ya kuwapa vyeti pekee.
Akizungumza
juzi kwenye sherehe za Mei Mosi zilizofanyika kimkoa wilayani Mkuranga,
Ndikilo alitoa siku tatu zinazoisha leo, taasisi hizo ziwe zimetekeleza
agizo hilo. Alisema walichofanya ni masihara na yeye hayuko tayari
kufanyiwa mzaha katika suala hilo, lililoandaliwa kwa muda mrefu.
“Katika
risala ya Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA)
Mkoa wa Pwani walilalamika kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya waajiri
kuwakopa zawadi za fedha watumishi wanaofanya vizuri kama motisha,” alisema.
Aliendelea,
“Lakini kwa hali hii siwezi kukubaliana nalo, nawapa siku tatu muwe
mmewalipa watumishi hao vinginevyo atakayeshindwa aje ofisini kwangu
akutane na adhabu niliyoiandaa.”
Alisema
hawezi kuvumilia watu wazembe wanaofanya dharau kwenye mambo mazito na
kwamba atachukua hatua kali kwa halmashauri ambazo zitashindwa kutoa
zawadi hizo kwani zingine zimetoa kwa nini wengine washindwe.
“Mimi
siyo mtani wenu, wala si saizi yenu, haiwezekani mniite nije kutoa
zawadi hewa, ndo maana hatua zikichukuliwa za kinidhamu mnasema
mnaonewa, ikifika Jumatano muwe mmeshawapa zawadi zao wahusika, huu ni
mzaha umepitiliza kiwango anayedhani tunatania aendelee aone,” alisema Ndikilo.
Licha
ya ofisi ya Katibu Tawala pamoja na Shirika la Elimu Kibaha, taasisi
nyingine zilizotakiwa kutekeleza agizo ni Halmashauri ya Wilaya ya
Bagamoyo, Halmashauri ya Mji Kibaha na Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji .
“Hatutaniani hapa,huu ni mzaha uliopitiliza kiwango,.ujumbe umefika.Namna
hii mnakatisha tamaa watumishi kwa kudai kuwa mchakato bado ni jambo
ambalo halijanifurahisha na nisingependa hali hii ijitokeze tena,” alisema Ndikilo.
Awali,
akisoma risala ya Tucta, Amini Msambwa alisema kuwa wafanyakazi wana
haki ya kutimiziwa haki zao za msingi na siyo lazima zipatikane kwa
shinikizo la maandamano, migomo na hata kufungia nje waajiri.
Msambwa
alisema kuwa moja ya changamoto ni baadhi ya wawekezaji wa nje na wa
ndani, kuwanyima fursa wafanyakazi kujiunga na vyama vyao sehemu za
kazi, ambayo ni haki yao ya kisheria na kwa kuzingatia kauli mbiu ya
mwaka huu ya Dhana ya Mabadiliko ilenge kuinua hali za wafanyakazi.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini