Wakati mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson
Kabwe ukitarajiwa kuzikwa Jumatano ijayo kijijini kwake Mamba, Mpinji
wilayani Same, chanzo cha kifo chake kimetajwa kuwa ni saratani ya tezi
dume na kuharibika kwa ini.
Kabwe
(pichani) alifariki dunia juzi alipokuwa akitibiwa katika Hospitali ya
Mama Ngoma, Mwenge Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Mauti
hayo yamemkuta ikiwa ni siku 38 baada ya kusimamishwa kazi hadharani na
Rais John Magufuli kwa tuhuma za kuingia mikataba iliyosababisha hasara
ya zaidi ya Sh3 bilioni.
Mtoto wa marehemu, Geofrey Kabwe, alisema baba yake alianza kuugua maradhi ya tumbo Julai mwaka jana.
Alisema Ilipofika Desemba, alizidiwa na familia iliamua kumpeleka India kwa matibabu zaidi.
“Alipofika
India waligundua kuwa alipata hitilafu ndogo kwenye ini, hivyo
akafanyiwa upasuaji, madaktari India walisema chanzo cha tatizo hilo ni
dawa alizokuwa akitumia,” alisema Geofrey.
Alisema
mwishoni mwa Januari, mkurugenzi huyo alirejea nchini akiwa na afya
njema na alianza kwenda kazini Februari huku akihudhuria kliniki katika
Hospitali ya Apollo nchini India.
Lakini
kadri siku zilivyozidi kwenda, hali yake kiafya ilianza kuzorota na
ilifikia hatua familia ilitakiwa kukutana ili kushauriana kuhusu hali
hiyo.
“Wiki
mbili zilizopita nilipigiwa simu nikiwa Arusha nikaelezwa kwamba hali
yake kiafya siyo nzuri, tulimwona daktari wake na akabainika kuwa na
Pneumonia (homa ya mapafu), akapewa dawa na sindano,” alisema Geofrey na
kuongeza: “Baadaye tulimpeleka TMJ kwa ajili ya kipimo cha CT-Scan,
jana mchana majibu yalitoka yakionyesha kuwa ini lilikuwa limeharibika
na tayari mwili ulikuwa umeanza kuvimba. Ilipofika saa mbili usiku hali
ilibadilika akawa anakoroma na saa tatu usiku akafariki dunia,” alisema
Geofrey.
Taarifa
zilizopatika jana zimeeleza kuwa Kabwe amekuwa nje ya ofisi yake tangu
alipoanza matibabu na siku ya kwanza kurejea kazini ilikuwa Aprili 19
ambako alikutana na rungu la Rais John Magufuli.
Mazishi
Msemaji
wa familia, Dk Ez Machuve alisema mipango ya mazishi inaendelea:
“Atasafirishwa kwenda kuzikwa nyumbani kwake Jumanne jioni baada ya
kuagwa hapa nyumbani kwake. Mazishi tunatarajia kufanya kijijini Mamba
Mpinji Jumatano.”
Meya
wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita alisema katika kipindi chake cha
kufanya kazi, hakubahatika kushiriki kazi yoyote na Kabwe kutokana na
hali yake kiafya. “Sikubahatika kufanya naye kazi, baada ya Rais kufanya
uamuzi mgumu, aliondoka hivyo sikuwahi kushiriki naye,” alisema Mwita.
Kilichomwondoa kazini
Makosa
yaliyosababisha Kabwe kusimamishwa kazi ni madai ya kusaini mkataba kwa
kutumia sheria ndogo ya mwaka 2004 kutoza magari yanayotoka kwenye
Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT) Sh4,000 huku akidaiwa kusaini
mkataba mwingine wa Sh8,000 chini ya sheria ndogo ya mwaka 2009.
Pia,
madai ya kukithiri kwa vitendo vya rushwa UBT hasa kwenye utaratibu wa
kutoa magari na kukodisha vyumba vya kupangisha kinyume na taratibu na
kuongeza muda wa mzabuni iliyeingia mkataba na jiji wa maegesho ya
magari kinyume na taratibu.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini