Chadema Walaani Wabunge wao wa Kike Kudhalilishwa Bungeni . | nyula blog

Habari Kila Pande

Breaking News
Loading...

Saturday, May 7, 2016

Chadema Walaani Wabunge wao wa Kike Kudhalilishwa Bungeni .


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Dar es Salaam kimelaani kauli iliyotolewa na Mbunge wa CCM, Goodluck Mlinga kuwa ili wanawake wapate nafasi ndani ya chama hicho lazima waitwe ‘baby’ neno linalomaanisha kutumiwa kimapenzi.

Hivi karibuni akichangia mjadala wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mlinga ambaye ni Mbunge wa Ulanga Mashariki alitoa kauli hiyo iliyoibua mtafaruku bungeni na kusababisha wabunge wanawake wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka nje ya ukumbi huo baada ya kunyimwa mwongozo na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.

Akizungumza jana nje ya eneo la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), akiwa na viongozi wenzake walipokwenda kuchangia damu, Katibu wa Chadema Dar es Salaam, Henry Kileo alisema wamesikitishwa na kauli hiyo ya mbunge aliyepewa dhamana na kuaminiwa wananchi.

Alisema ili uwe mbunge wa viti maalumu ndani ya Chadema, kuna hatua nne za kupitia ikiwamo wanawake wenyewe kuchaguana ngazi ya wilaya kupitia Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), hivyo siyo rahisi kuwa na kitu kama hicho cha uhusiano wa kimapenzi.

Kileo alisema: ‘‘Lakini cha ajabu nimeshangaa hata wenzetu upande wa pili CCM wamekaa kimya bila kutoa kauli ya kukaripia.’’

Alisema Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, inaungana na wabunge wanawake wa Ukawa kupinga kauli hizo za kihuni.

Kuhusu suala la damu, Kileo aliwataka Watanzania kujenga tabia ya kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wengine waliolazwa katika hospitali na vituo vya afya nchini.

“Chadema Dar es Salaam, tumeonyesha mfano tunaviomba vyama vingine viige mfano huu ili tuwasaidie watu wenye mahitaji ya damu,” alisema Kileo.

Alisema zaidi ya wanachama 40 wakiwamo viongozi wa Chadema wamechangia damu na kwamba mchakato huo utakuwa wa mara kwa mara.

Mbunge wa VitiMaalumu, Ruth Molel alisema wabunge wa Chadema wanaoteuliwa wana taalumu zao na hawabahatishi kupata nafasi hizo kama Mlinga anavyodhani.

“Nimeumia nilivyosikia kauli hii ikitolewa na kijana yule ambaye ni kama mwanangu, kiukweli hajatutendea haki kina mama.Inaonyesha jinsi gani bado ana fikra za mfumo dume,”alisema Molel.

Ofisa Habari wa MNH, Neema Mwangomo alisema kwa siku hospitali hiyo inahitaji damu kwa wastani uniti 80 hadi 100 lakini zinazopatikana ni 40.

Hata hivyo, Mwangomo aliwashukuru viongozi Chadema kwa moyo wao na kuwataka Watanzania wengine kujitokeza kutoa damu katika hospitali hiyo.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin