Baadhi
ya vyombo vya habari vimekuwa vinatoa taarifa potofu kuhusu mchakato
wa Mwenyekiti wa sasa wa CCM Dkt. Jakaya Kikwete kukabidhi kijiti cha
uongozi wa CCM kwa Rais John Pombe Magufuli kama ilivyo mila na desturi
ya Chama Cha Mapinduzi. Yamekuwepo madai eti Mwenyekiti amekataa au
anachelewesha kukabidhi kijiti.
Habari
hiyo sio kweli kabisa na ni kinyume chake, kwani Dkt. Kikwete amekuwa
akisisitiza kukabidhi madaraka mapema iwezekanavyo.
Kwa
ajili hiyo kwenye kikao cha Mei 3, 2016 alikataa kusiongezwe agenda
nyingine ambazo zitalazimisha Mkutano Mkuu Maalum kuchelewa kufanyika
kwa sababu ya kukamilisha maandalizi ya agenda hizo. Alisisitiza agenda
iwe moja tu.
Dhamira ya kufanyika Mkutano Mkuu maalum mwezi Juni, 2016 iko pale pale. Kilichoelezwa kwenye kikao ni kutaka kukamilisha utaratibu wa kupata fedha za kugharamia mkutano huo. Taratibu zikikamilika tarehe itapangwa. Mipango ya kutafuta pesa inaendelea na ikikamilika tarehe itatangazwa.
Tunawataka
wana-CCM wasihamanike wala kubabaishwa na taarifa za upotoshaji
zinazofanywa na watu wenye nia mbaya na CCM. Hawa ni wale wale ambao
wamekuwa wakiiombea mabaya CCM bila ya mafanikio.
Pia
tunapenda kukanusha madai ati kuwa Mwenyekiti Kikwete aliwatahadharisha
Wajumbe wa Kamati Kuu kuhusu ukimya wa Ndugu Edward Lowassa. Hakuna
wakati wowote kauli kama hiyo aliitoa. Ni uzushi mtupu. Jina la Ndugu
Lowassa halikutajwa kabisa.
Aidha,
tunapenda kukanusha madai ya kufanyika mkutano baina ya Mwenyekiti wa
CCM, Rais wa Jamhuri ya Muungano, Makamu wa Rais na Katibu Mkuu wa CCM
kuhusu uchaguzi wa Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM.
Hapajawahi
kufanyika mkutano wa aina hiyo siku yoyote na mahali popote. Hivyo
madai ya kuwepo kwa tofauti baina ya Viongozi wakuu kuhusu nani
achaguliwe kuwa Katibu wa Wabunge wa CCM hayana msingi wowote.
Kamati
Kuu iliteua Wabunge wanne kugombea na kuwaachia Wabunge wa CCM kuamua.
Kuhusisha Viongozi na hasa kuzua kuwepo kutokuelewana ni jambo la
kusikitisha. Ni taarifa ya uongo yenye nia ovu kwa CCM na Viongozi wake.
Tunapenda
kuwatahadharisha waandishi wa habari kuandika habari za ukweli. Waache
kuzua mambo yenye kupandikiza chuki na mgawanyiko usiostahili kuwepo
ndani ya CCM na kuyaeneza kwa watu. Waheshimu maadili ya kazi zao.
Napenda kuwahakikishia na kusisitiza kuwa hakuna mgogoro wa kukabidhi kijiti cha uenyekiti katika CCM na wala hautakuwepo.
Imetolewa na;
Ndugu Christopher Ole Sendeka
MSEMAJI WA CCM
MJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
05/05/2016
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini