CCM Waituhumu Chadema Arusha Kugawa Miradi Kwa Kupendelea Maeneo Waliyoshinda . | nyula blog

Habari Kila Pande

Breaking News
Loading...

Wednesday, May 25, 2016

CCM Waituhumu Chadema Arusha Kugawa Miradi Kwa Kupendelea Maeneo Waliyoshinda .


CCM Mkoa wa Arusha, imeziomba halmashauri tano kati ya saba zinazoongozwa na Chadema, kugawa miradi ya maendeleo kwa usawa katika maeneo yao ili kuunga mkono msimamo wa Rais John Magufuli wa kuhudumia wananchi bila ubaguzi wa itikadi za vyama.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Michael Laizer alitoa kauli hiyo jana katika mkutano na viongozi wa chama hicho na Serikali katika kata za Lolksale na Lemoot wilayani Monduli, wakati wa ziara yake ya kuhamasisha utekelezaji wa ilani ya CCM na kukiimarisha chama hicho. 

Alisema katika halmashauri zinazoongozwa na upinzani alikopita amegundua kuwapo kwa utoaji wa miradi usio na uwiano, kwa kubagua baadhi ya kata zinazoongozwa na madiwani wa chama tawala, hali inayoweza kuzua malumbano.

Hata hivyo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Calist Lazaro alisema malalamiko hayo ya CCM hayana msingi kwa kuwa madiwani wa chama hicho katika halmashauri zote wanajua wajibu wao na hakuna upendeleo wowote.

Lazaro ambaye pia ni Meya wa Jiji la Arusha, alisema CCM haitengwi kwani haina uongozi katika kata nyingi. Alisema kati ya kata 24 CCM imeshinda moja, hivyo wanapoona kazi zinafanyika kwenye kata hizo wanadhani ni upendeleo.

Madai ya Laizer 
Mwenyekiti huyo wa CCM alisema viongozi wa Chadema wanaoendekeza siasa hadi sasa baada ya uchaguzi kumalizika, hawatendi haki kwa kuwa kuchagua au kuchaguliwa ni hiari ya kila mtu na kamwe mwananchi hapaswi kuhukumiwa kwa uamuzi aliofanya kidemokrasia.

“Kwa nini wao viongozi wa chini wanaendekeza ubaguzi wakati kiongozi mkuu wa nchi ambaye ni Rais anaendelea kusisitiza kutoa huduma kwa wananchi pasipo na ubaguzi?” alihoji na kuongeza:

“Kama Rais Magufuli angeamua kuzinyima fedha baadhi ya halmashauri zinazoongozwa na vyama vya upinzani, kungekuwa na madhara makubwa hivyo wapinzani wajirekebishe.”

Laizer aliwataka wananchi wa kata na halmashauri hizo zinazokabiliwa na matatizo hayo, kutokuwa wanyonge kwa kuwa wanaye baba ambaye ndiye Rais anayeonyesha hana ubaguzi na wala si muumini wa masuala ya vyama vya siasa, baada ya yeye kuchaguliwa kushika wadhifa huo.

Mwenyekiti huyo anaendelea na ziara wilayani Monduli ikiwa ni wilaya yake ya nne, baada ya kupita katika wilaya za Meru, Arumeru na Karatu kwa kazi hiyo ya uhamasishaji wa utekelezaji wa ilani ya chama chake.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin