Malori
ya kubeba mizigo, ambayo yamekuwa yakichangia msongamano wa magari kwa
kiasi kikubwa jijini Dar es Salaam, yanatarajiwa kuondolewa mara tu reli
ya kisasa ‘Standard Gauge’, iliyotengewa Sh trilioni moja katika Bajeti
ya Serikali, itakapofika Ruvu mkoani Pwani.
Rais
John Magufuli amesema hayo jana wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi
wa barabara ya kwanza ya juu (Flyover) nchini Tanzania, inayojengwa
katika makutano ya Barabara ya Mandela na Barabara ya Nyerere eneo la
Tazara, kwa ufadhili wa Serikali ya Japan.
Barabara
hiyo ya juu kwa mujibu wa taarifa za Wakala wa Barabara (Tanroads),
ikikamilika inatarajiwa kupunguza muda wa magari kukatiza katika
makutano hayo kwa asilimia 80, kutoka wastani wa dakika 45 hadi dakika
10 tu kwa wanaotoka upande mmoja kwenda mwingine.
Akifafanua
zaidi kuhusu reli, Rais Magufuli alisema fedha hizo zimetengwa katika
bajeti itakayopelekwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
linalotarajiwa kuanza vikao vyake wiki ijayo, ili ujenzi uanze kwa fedha
za ndani wakati wafadhili wa kusaidia kuendeleza wakitafutwa na
wakipatikana, wakute reli hiyo imeanza kujengwa.
Kwa
mujibu wa Rais Magufuli, reli hiyo itakapofika Ruvu, kutajengwa bandari
kavu kubwa ambayo ikikamilika, mizigo yote inayoshuka Bandari ya Dar es
Salaam, itasafirishwa kwa reli mpaka katika bandari hiyo na malori
yanayochukua na kupeleka mizigo katika bandari hiyo, yataishia katika
bandari hiyo kavu.
Ili
kuepuka wizi wa mizigo, Rais Magufuli alisema kutafungwa kamera katika
njia yote ya reli mpaka Ruvu, ili kontena linaloshushwa katika Bandari
ya Dar es Salaam, lifuatiliwe mpaka katika bandari hiyo.
Mbali
na reli hiyo ambayo ikikamilika kwa mujibu wa taarifa za Mamlaka ya
Bandari (TPA), itapunguza gharama za usafirishaji wa mizigo kwa asilimia
30 na kuongeza kivutio cha bandari hiyo duniani, Rais Magufuli alisema
Mfuko wa Barabara utatoa fedha za kujenga barabara za pete,
zitakazoongeza kasi ya kupunguza msongamano kama si kuumaliza.
Alionya
kuwa fedha za Mfuko wa Barabara si za kulipana posho, bali kutengeneza
barabara hizo za pete katika halmashauri na kuagiza makandarasi wanaotoa
asilimia 10 kwa ajili ya rushwa, wasipewe zabuni bali watafute
makandarasi wazuri.
Alisema
kilometa 27 za barabara hizo za pete, zimeanza kujengwa na kwa kuwa
wabunge wa Dar es Salaam waliopita walisema sana, waliongezewa kilometa
nyingine 86 za barabara hizo za pete, zitakazojengwa kwa lami kwa fedha
za mfuko huo.
Malori kutaifishwa
Pia
Rais Magufuli ameagiza halmashauri za Dar es Salaam kuweka sheria
itakayokataza kupitisha magari yenye tani zaidi ya 56 katika barabara
hizo, yakiwemo malori ili barabara hizo zilizokusudiwa kutumika na
magari madogo, zisiharibiwe na magari yenye uzito mkubwa.
“Hakuna
kupitisha magari yenye tani zaidi ya 56 na mtu akipitisha kamateni gari
na ikiwezekana litaifishwe kabisa ili ajifunze kutopita katika barabara
hizo na kuziharibu,“ alisisitiza.
Akizungumzia
miradi hiyo ya kupunguza msongamano ikiwemo barabara za juu ikiwemo ya
Ubungo, Rais Magufuli alisema zitapunguza hasara iliyokuwa ikitokea
kwani katika utafiti wa mwaka 2013, ulionesha kuwa Jiji la Dar es Salaam
pekee lilipoteza Sh bilioni 411.3 katika msongamano wa magari.
Mbali
na hasara hiyo iliyooneshwa katika utafiti, Rais Magufuli alisema
inawezekana kabisa msongamano wa magari Dar es Salaam umesababisha
baadhi ya watu kufa kwa kuchelewa kufikishwa hospitalini na baadhi ya
ndoa kuvunjika kutokana na kuchelewa kufika nyumbani na kushindwa
kujieleza.
Rais
alisema msongamano ni tatizo na kama siyo kumaliza basi lazima
lipunguzwe kabisa kwa kuwa Dar es Salama ndiyo kioo cha Tanzania, ambapo
mizigo inayotoka na kwenda nchi zisizo na bandari inapita hapo.
Alisema
barabara ya juu ya Tazara, itatengeneza ajira nyingi na asilimia kubwa
ya wanufaika watakuwa Watanzania tena wakazi wa Jiji la Dar es Salaam,
akawaomba vijana watakaopata ajira kwenye mradi huo, kufanya kazi kwa
uaminifu wasiibe mafuta, vifaa na wasigome ili umalizike mapema.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini