Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amekumbana na joto la Mbeya baada ya
meya wa jiji hilo, Mchungaji David Mwashilindi na madiwani wake 34
kususia kikao chake cha kujitambulisha kwa wananchi, baada ya kudaiwa
kwenda kukagua Soko la Mwanjelwa bila kumpa taarifa yoyote meya wa jiji
hilo.
Meya alifikia uamuzi huo ndani ya ukumbi wa Mkapa muda
mfupi kabla ya Makalla kuanza kuzungumza na watumishi wa jiji, wananchi,
wazee maarufu, viongozi wa dini na machifu ambapo Mkuu wa Wilaya ya
Mbeya Nyirembe Sabi alimkaribisha Meya Mwashilindi kuzungumza chochote
kwa niaba ya madiwani wake.
Hata hivyo, Meya Mwashilindi
alipochukua kipaza sauti alisema: “Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, nakumbuka kwa
mara ya kwanza kukutana na wewe tulizungumza kwamba tufanye kazi, siasa
zimekwisha. Lakini masikitiko yangu ni kwamba leo hii umekwenda Soko la
Mwanjelwa bila ya mimi mwenye jiji kupewa taarifa yoyote wala madiwani
wangu. Sasa hiki kikao hakinihusu hivyo muendelee na kikao chenu.”
Baada
ya kusema maneno hayo alikabidhi kipaza sauti kwa mkuu wa wilaya, kisha
akachukua nyaraka zake akainuka pamoja na madiwani wote kupitia Chadema
na kutoka ukumbini huku wakisikika wakisema, ‘hizi ni siasa ambazo
tulizikataa, lakini wanatulazimisha kuendesha siasa. Hatuwezi kupuuzwa
kwa kiasi hiki.”
Mkuu wa Wilaya, Mnasa alisema anaamini taratibu
na ratiba yote ilipangwa vizuri hivyo hawaoni sababu ya madai ya
madiwani hao kwamba hawakushirikishwa kwenye ziara hiyo, wao kama
wawakilishi wa Rais hawaangalii siasa, bali wanaangalia uchapakazi na
siyo masuala ya siasa.
Akizungumzia kitendo cha meya na madiwani
wake kususia kikao hicho, Makalla alisema ‘Nashangazwa na uamuzi wa
madiwani hawa kwa kitendo hiki, kwani siku ile nilipotembelea Shule ya
Sekondari Iyunga, nilisema kwamba Aprili 20 ambayo ndiyo leo (jana)
nitakuwa na ziara ya jiji na kabla ya kikao nitataka kutembelea Soko la
Mwanjelwa,” alisema Makalla.
Alisema suala la meya na madiwani
wake kutoshirikishwa kwenye ziara ya kwenda Soko la Mwanjelwa halimhusu,
kwani mwenye wajibu wa kupeana taarifa ni kwenye ngazi ya halmashauri
ya jiji, lakini siyo yeye (Makalla).
“Jamani mimi sijaja kufanya
siasa nimekuja kufanya kazi ya wananchi na nilishatahadharisha jambo
hili, sasa kwa kitendo hiki ndiyo siasa na wananilazimisha kufanya
siasa, lakini wao ndiyo watahukumiwa na wananchi. Na ninasema kama Mola
ataendelea kunilinda kubaki katika mkoa mwaka 2020 nitakwenda kuwaambia
hiki kinachofanyika sasa na wawakilishi wao,” alisema Makalla.
Awali
Makalla akiwa katika Soko la Mwanjelwa alinusa harufu ya ufisadi kwenye
soko hilo na kuagiza vyombo vya ulinzi na usalama mkoa huo, kufanya
uchunguzi ndani ya wiki nne wa uhalali wa fedha kiasi cha Sh22.9 bilioni
iliyotumika katika ujenzi huo ukiwa ni mkopo kutoka Benki ya CRDB.
Makalla
alitoa agizo hilo jana mchana baada ya kutembelea soko hilo na
kuzungumza na wafanyabiashara wa jijini hapa, ambao walimueleza
wanashindwa kumudu gharama ya upangaji ya vyumba vya biashara ambayo
inaanzia kiasi cha Sh500,000 kwa chumba kimoja kwa mwezi, ndiyo maana
hawataki kuingia ndani ya soko hilo.
Mwenyekiti wa soko hilo,
Peter Chacha alimueleza Makalla kwamba wasipokuwa makini soko hilo
litabaki gofu, kwani wafanyabiashara hawataki kuingia kwa kuogopa
gharama kubwa ya vyumba hivyo, alimuomba afanye awezalo kukaa chini na
uongozi wa benki ambao unadai fedha zao kwa jiji na kuona namna ya
kupunguziwa gharama hiyo.
“Ni kweli wenzetu jiji, wametingwa na
deni la mkopo kutoka Benki ya CRDB, ndiyo maana wamekuja kutubana sisi
wafanyabiashara kwa kutupangia chumba kuanzia Sh500, 000 hadi Sh
800,000, kitu ambacho hatuwezi kumudu hata kidogo,”alisema
Chacha
Baada ya kusikiliza kilio cha wafanyabiashara hao, Makalla
alisema kiasi cha Sh22.9 bilioni iliyotumika kwenye ujenzi wa soko hilo
haiendani na thamani yake, hivyo vyombo vya dola vikiongozwa na Kamanda
wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mbeya,
wanafanya uchunguzi wa kina na kuwanasaka wale wote waliohusika kwenye
mchakato mzima wa ujenzi wa soko hilo.
“Nataka kupata taarifa ya
mchanganuo mzima wa namna ya fedha ilivyokopwa, ilivyotumika na mkataba
wake ulivyokuwa ndani ya wiki nne, taarifa hii niipokee na wale
watakaobainisha kufuja fedha watapelekwa mahakamani kwa mujibu wa
sheria.
"Kwenye hili, kuna watu waliotufikisha hapa, Sh22.9
bilioni iliyotumika kwenye ujenzi huu haiendani na ujenzi wa soko hili,
kuanzia muda uliotumika na gharama ya kodi ya upangishaji wa vyumba siyo
rafiki ni kubwa mno, hivyo jiji na CRDB mkae muone namna ya kupunguza
gharama hiyo, kwani hali ilivyo sasa lile soko litabaki gofu."
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini