Serikali
imetoa jumla ya Sh. Bilioni 318.406 kwa mwezi wa Januari mwaka 2016,
kwa ajili ya miradi ya maendeleo nchini na Sh. Bilioni 538.5 kwa
mishahara ya watumishi wa Umma.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya
Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Servacius Likwelile
alisema kuwa Serikali inajivunia kufanikiwa kutumia fedha za ndani kwa
ajili ya miradi ya maendeleo ambapo hadi sasa Serikali imetumia kiasi
cha Sh. Bilioni 71.2 tu kutoka fedha za nje.
Dkt.
Likwelile alisema mapato yanayokusanywa nchini yamewezesha kutekeleza
sera ya elimu bure ambapo mwezi Desemba mwaka 2015 Serikali ilitoa
kiasi cha Sh. Bilioni 18.77 kwa shule za msingi na sekondari kwa ajili
ya ruzuku, ada na chakula kwa shule za bweni pamoja na mahitaji mengine
ambapo mwezi wa Januari 2016 Serikali imetoa kiasi cha Sh. Bilioni 18.77
kwa ajili ya kutekeleza Sera hiyo.
Aliongeza
kuwa katika ulipaji wa madeni ya wakandarasi nchini , Serikali imetoa
Sh. Bilioni 130 kwa mwezi Januari mwaka 2016 ambapo mwezi Desemba mwaka
2015 ilitoa Sh. Bilioni 193.
Kwa
upande wa Mfuko wa Barabara, Katibu Likwelile alifafanua mradi huo
umetengewa kiasi cha Sh. Bilioni 47.89 na kuongeza kuwa Benki kuu ina
fungu la mfuko huo ambapo nayo imetenga kiasi cha Sh. Bilioni 76.3.
Dkt.
Likwelile alisema kuwa Halmashauri zitapelekewa kiasi cha Sh. Bilioni
20.52 kwa ajili ya kuboresha barabara na jumla mfuko huo kufikia kiasi
cha Sh. Bilioni 274.71.
Akifafanua
kuhusu miradi ya umeme, Dkt. Likwelile alisema kuwa mwezi Desemba mwaka
2015 Serikali ililipa deni la TANESCO kiasi cha Sh. Bilioni 80 za mradi
wa Kinyerezi II na kwa mwezi Januari mwaka 2016 kiasi cha Sh. Bilioni
40 zimetengwa kwa ajili ya mradi huo.
Hali hii imefikisha kiasi cha Sh. Bilioni 120 kwa ajili ya kulipa madeni na kuendeleza uzalishaji wa umeme nchini.
Alisema
kiasi cha Sh. Bilioni 21.959 kimetengwa kwa ajili ya mradi wa umeme
vijijini na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ina mfuko wa mradi huo ambao kwa
sasa una kiasi cha Sh. Bilioni 21.9 na kuongeza kuwa huduma ya umeme
kwa wananchi itaimarika.
Alifafanua
kuwa Serikali imeanzisha mfuko wa maji Benki Kuu ya Tanzania (BoT)
ambapo mpaka sasa mfuko huo una jumla ya kiasi cha Sh. Bilioni 46.3.
Aidha,
BoT imetoa Sh. Bilioni 12.5 kuendeleza miradi ya maji ambapo kwa
Januari mwaka 2016 Serikali imetenga kiasi cha Sh. Bilioni 7.7.
Serikali
imetenga kiasi cha Sh Bilioni 82.2 kwa mwezi wa Januari ili kuweza
kulipa pensheni za wastaafu, na kwa wale wastaafu walio katika daftari
la kudumu ambapo wametengewa kiasi cha Sh. Bilioni 33.3 kwa ajili ya
malipo yao.
Wabunge
wametengewa kiasi cha Sh. Bilioni 35.5 kwa ajili ya mkopo wa magari
ambapo kila mbunge atapata kiasi cha Sh. Milioni 90, kiasi cha Sh.
Milioni. 45 ni ruzuku na Sh. Mil. 45 ni mkopo ambao utalipwa ndani ya
miaka 5.
Aidha, Serikali imetenga kiasi cha Sh. Bilioni 784.3 kwa ajili ya kulipa deni la taifa.
Naye
Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata alibainisha
kuwa hali ya makusanyo ya mapato nchini iko vizuri ambapo kwa mwezi
Januari 2016, makadirio yalikuwa Sh. Trilioni 1 na Bilioni 45 na hadi
kufikia sasa kiasi cha Sh. Trilioni 1 na Bilioni 31 zimeshakusanywa.
Matarajio ya TRA ni kukamilisha kukusanya kiasi cha Sh. Billioni 14 zilizosalia.
Aidha,
Kidata alibainisha kuwa uingizaji wa bidhaa kupitia bandarini bado uko
vizuri licha ya minong’ono kuwa uzuiaji wa mianya ya ukwepaji kodi
imepunguza uingizaji bidhaa ambapo kwa mwezi Januari Bilioni 111
zimekusanywa kutokana na ushuru wa forodha.
Kidata alitoa wito kwa kila mtanzania kulipa kodi na kutoa taarifa za wakwepa kodi ili kuweza kukuza mapato ya nchi.
Kwa
upande wake Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Benno Ndulu
amepongeza juhudi za ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa matumizi ya
fedha za Serikali.
Alisema
kuwa uchumi umekua na unazidi kuimarika licha ya changamoto za kiuchumi
duniani ambapo uchumi wa nchi umekua kwa asilimia 7 na unategemewa
kukua miezi ijayo kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji nchini.
Mfumuko
wa bei unaendelea kubaki ndani ya kiwango cha tarakimu moja, licha ya
ongezeko dogo katika miezi ya hivi karibuni kutokana na kupanda kwa bei
za vyakula.
Alisema
kuwa mfumuko wa bei ulikuwa asilimi 6.8 mwaka 2015, ukilinganishwa na
asilimia 6.1 kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 2015.
Wakati
huo huo mfumuko wa bei usiojumuisha chakula na nishati uliendelea
kubaki katika viwango vya chini ya asilimia 2.5 kutokana na hatua
mbalimbali za kisera zilizochukuliwa na BoT.
Prof.
Ndulu alifafanua mapato ya fedha za kigeni yanaendelea vizuri ingawa
bei ya dhahabu imeshuka kutoka Bilioni 2.5 hadi Bilioni1.3.
Sekta ya utalii imesaidia kuimarisha fedha za kigeni kwani mapato yameongezeka kutoka Bilioni 1.5 hadi Bilioni 2.2.
Sekta
ya viwanda nayo imeshika nafasi ya pili katika kuongeza fedha za kigeni
nchini ambapo mwaka 2015 mapato yalikuwa Bilioni 1 na kwa sasa
yamefikia Bilioni1.5.
Aidha,
Prof. Ndulu aliongeza kuwa sekta ya usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi
imesaidia kuimarisha fedha za kigeni ambapo mapato yamefikia Dola
Bilioni11 kwa mwaka.
Hadi kufikia sasa Tanzania imenufaika kutokana na kupungua kwa bei ya mafuta katika uingizaji bidhaa hiyo kwa asilimia 44.
Serikali inatarajia kuendelea kuimarisha uchumi ili kufikia azma ya kuwa nchi ya uchumi wa kati hadi ifikapo 2025.
Imetolewa na Wizara ya Fedha na Mipango
Kitengo cha Mawasiliano
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini