KATIBU
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest
Rwegasira amewataka viongozi wakuu wa Jeshi la Polisi nchini kuhakikisha
wanawachukulia hatua kali askari polisi wenye tabia ya kuwabambikizia
kesi wananchi.
Meja
Jenerali Rwegasira alisema Jeshi hilo lina sifa nzuri nje ya nchi
pamoja na hapa nchini lakini kuna baadhi ya askari wasiowaadilifu
wanawaonea wananchi mitaani wasiokuwa na hatia kwa kuwabambikizia kesi
ambapo wanalitia doa jeshi hilo.
“Jeshi
letu lina sifa nzuri, niliwahi kwenda nchini Kenya nikaambiwa Jeshi la
Polisi Tanzania lina maadili kwani hata likimkamata mhalifu linafuata
sheria na utaratibu na sio kutumia nguvu kubwa kama yalivyo majeshi
mengine,” alisema Rwegazira.
Rwegasira
aliongeza kuwa, amefurahishwa sana na utendaji kazi wa jeshi hilo na
kutaka kuongeza umakini zaidi ili kuliletea sifa zaidi jeshi hilo na
yeye yupo karibu nao katika kuliendeleza jeshi hilo ili liweze kufanya
kazi kwa weledi.
Alisema
kuwa ni askari wachache mno wenye tabia hiyo ya kuwabambikizia kesi
wananchi na kutofuata sheria za jeshi, hivyo kazi ya kupambana na askari
hao inawezekana endapo viongozi wa jeshi wakiamua kulifanyia kazi.
“Utendaji
kazi wenu ni mzuri, nawapongeza sana hasa mlivyosimamia uchaguzi mkuu
vizuri kwani wananchi wengi walikuwa na wasiwasi kuhusu usalama wao
katika kipindi cha uchaguzi, lakini mlisimama imara kuhakikisha uchaguzi
unamalizika salama,” alisema Rwegasira.
Hata
hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Simba Yahya naye alitoa
pongezi kwa jeshi hilo na kuwataka kuyapeleka mahitaji yao katika ofisi
ya Katibu Mkuu pamoja na yeye ili waweze kuyafanyia kazi na hatimaye
kuliboresha jeshi hilo.
Kwa
upande wake Mkuu wa Jeshi hilo nchini, IGP Ernest Mangu aliwapongeza
Viongozi hao wa Wizara kwa kuwatembelea katika ofisi za Makao Makuu ya
Jeshi kwani wamefarijila na kuwahakikishia viongozi hao kuwa wamejipanga
vizuri katika kulinda usalama wa raia na mali zao na watayafanyia kazi
maagizo waliyopewa.
Katibu
Mkuu pamoja na Naibu wake wanamekamilisha ziara yao ya kuzitembelea
Idara za Wizara hiyo ambazo ni Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Idara
ya Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Mamlaka ya Vitambulisho
vya Taifa (NIDA), ambapo lengo la ziara hizo ni kujitambulisha kwa
viongozi hao pamoja na kujifunza kazi mbalimbali zinazofanywa na idara
hizo.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini