
MBUNGE
wa Bariadi, Andrew Chenge na wabunge wawili wa Viti Maalumu, Dk Mary
Mwanjelwa na Najma Giga, wamechaguliwa kuwa Wenyeviti wa Bunge kwa
kipindi cha miaka miwili na nusu.
Uchaguzi
huo ulifanyika jana baada ya majina yao kupendekezwa na Kamati ya
Uongozi na kuyawasilisha bungeni kwa ajili ya uchaguzi.
Katika
uchaguzi huo, uliotanguliwa na wabunge hao kujieleza mbele ya wenzao na
kuulizwa maswali, sakata la Tegeta Escrow liliibuka baada ya Chenge
kujieleza.
“Katika
Bunge lililopita, chama chako na wabunge walikuwajibisha kwa kashfa ya
Escrow, je, siku ukiliongoza Bunge na hoja ikarudi ndani uko tayari
kuisimamia,” Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe (Chadema) alimuuliza Chenge.
Akijibu
swali hilo, Chenge alisema Bunge linaongozwa na Kanuni na itakapokuja
mbele ya Bunge au kwenye Kamati, ikaonekana kuna maslahi ama inamhusu
mbunge, ni busara kuzingatia kanuni nafasi hiyo ikaachwa mwingine
aifanye shughuli za Bunge zisiwe na makandokando ya aina yoyote.
“Naona niishie hapo, ningeweza kusema zaidi ya hapo,”
alisema Chenge ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa zaidi ya
miaka 10 na pia Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la 10 kabla ya
kujiuzulu kutokana na sakata la Tegeta Escrow.
Awali akijieleza Chenge ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, alisema “napenda niliahidi Bunge na Watanzania kwa ujumla, kwamba hii ni dhamana nzito ya kumsaidia Spika na Naibu.
“Lakini
niwahakikishie nitatekeleza jukumu hilo kwa uadilifu, na kwa uaminifu
ili nitende haki inayoonekana na bila chuki, wala upendeleo wowote kwa
faida ya kujenga misingi bora ya Bunge hili lakini pia kwa kuwatumikia
Watanzania wote,” alisema.
Kuhusu
swali la Mbunge wa Nsimbo, Richard Mbogo (CCM) aliyetaka kufahamu ni
namna gani Chenge atadhibiti matumizi ya lugha ya kuudhi au kudhalilisha
wengine, Chenge alisema Kanuni za Bunge kama zilivyo sheria za nchi,
zinakata pande zote kama ilivyo msumeno.
Alisema ikithibitika kwamba mbunge amekiuka kanuni, kiti kitazingatia baada ya kupima kauli na maelezo aliyotoa bungeni.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini