Kampuni ya kufua umeme ya Symbion imesema maneno ya uzushi na ukiukwaji
wa mikataba unaofanywa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)
utaligharimu Taifa na kulitaka shirika hilo kusema ukweli kuhusu
makubaliano yao.
Kampuni hiyo pia imeeleza kuwa mwishoni mwa
mwaka jana, kigogo mmoja wa Tanesco (ametajwa jina lakini tunalilisitiri
jina lake kwa sababu hakupatikana jana) alisaini mkataba na Symbion wa
kuliuzia umeme shirika hilo la umma kwa miaka 15.
Taarifa
iliyoletwa jana kwa vyombo vya habari na mshauri wa Symbion, Julius
Foster inaeleza kuwa taarifa zote zinazotolewa na Tanesco kuhusu
uhusiano wao wa kimkataba ni za uongo na zimewashtua kwa kuwa shirika
hilo la Serikali halijawahi kuieleza Symbion kuhusu tuhuma hizo.
“Kama
itatokea suala hili likaleta mgogoro wa kitaifa, tunataka Tanesco na
Serikali na yeyote yule kufafanua masuala haya kwa kiapo na mbele ya
mahakimu na tutaujulisha umma kila kitu,” inasema taarifa hiyo.
“Zaidi
ya barua ambayo walitaka kusitisha majadiliano na Symbion, hajawahi
kujadili na sisi jambo lolote ambalo (kigogo huyo wa Tanesco),
analizungumza sasa kwenye vyombo vya habari huko Tanzania.”
Hivi
karibuni, iliripotiwa kuwa Tanesco imepanga kufungua kesi ili kusitisha
mkataba na Symbion kutokana na wingi wa kesi dhidi ya kampuni hiyo ya
Kimarekani.
Miongoni mwa kesi hizo ni ile iliyofunguliwa
Mahakama ya Biashara na East African Cables dhidi ya Symbion Tanzania
Ltd kutokana na deni la Sh6.372 bilioni. Tanesco ina hisa kwenye kampuni
ya East African Cables.
Kadhalika, taarifa hizo zinaeleza kuwa
Tanesco imeamua kusitisha mkataba huo kutokana na Symbion kudaiwa Sh6
bilioni na kampuni ya Oilcom, yakiwa ni malimbikizo ya malipo ya
usambazaji wa mafuta kwa miaka mitatu.
Hivi karibuni, Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema mikataba yote ya
Tanesco na kampuni za kufua umeme si mizuri na haina manufaa yoyote kwa
Taifa.
Akijibu swali bungeni, Profesa Muhongo alikiri kwamba
deni la Tanesco ni kubwa na limesababishwa na uongozi dhaifu, rushwa,
wizi na mikataba mibovu ambayo Tanesco imeingia. Alisisitiza kwamba
hakuna mkataba unaolinufaisha Taifa.
Taarifa ya Symbion inaeleza
kuwa wakati Tanesco inataka kusitisha mkataba huo, imeshindwa kulipa
kiasi cha kati ya dola 25 milioni za Marekani na dola 80 milioni katika
kipindi cha miaka mitano.
“Pamoja na deni hilo katika kipindi
cha miaka mitano, hatukuwahi kuzima umeme, tukaendelea kuzalisha umeme
na kujenga vituo vya dharura vya kufua umeme kwa kuwa kama si hivyo,
Tanzania ingeingia gizani kwa sababu kiwango cha maji cha Mtera, Kihansi
na Kidatu kilikuwa chini,” inasema taarifa hiyo.
“Kwa kuwa sasa mabwawa yamejaa ndiyo mnataka kuvunja mkataba?
“Tukifanya
hivyo, wanaoathirika ni Watanzania. Tuna uhakika baadhi ya vigogo wa
Tanesco hawaathiriki kwa sababu wana jenereta, ni wananchi ndiyo
wanaoathirika.”
Taarifa hiyo inasema pamoja na kauli ambazo
imeziita za uzushi zinazotolewa na shirika hilo, bado Symbion inasubiri
majibu ya barua ambayo iliituma kwa Serikali wiki tatu zilizopita kuhusu
mkataba huo.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini